| Chapter 27 |
1 | Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumwua. |
2 | Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa. |
3 | Hapo, Yuda ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu zile sarafu thelathini za fedha. |
4 | Akawaambia, "Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe." Lakini wao wakasema, "Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako." |
5 | Naye akazitupa zile fedha Hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga. |
6 | Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, "Haifai kuziweka katika hazina ya Hekalu kwa maana ni fedha za damu." |
7 | Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. |
8 | Ndiyo maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu. |
9 | Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: "Walizichukua sarafu thelathini za fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walipanga bei, |
10 | wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza." |
11 | Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, "Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?" Yesu akamwambia, "Wewe umesema." |
12 | Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno. |
13 | Hivyo Pilato akamwuliza, "Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?" |
14 | Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana. |
15 | Ilikuwa kawaida wakati wa Sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka. |
16 | Wakati huo kulikuwa na mfungwa mmoja, jina lake Baraba. |
17 | Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, "Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba*fq* ama Yesu aitwae Kristo?" |
18 | Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu. |
19 | Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: "Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake." |
20 | Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe. |
21 | Mkuu wa mkoa akawauliza, "Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?" Wakamjibu, "Baraba!" |
22 | Pilato akawauliza, "Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?" Wote wakasema, "Asulubiwe!" |
23 | Pilato akauliza, "Kwa nini? Amefanya kosa gani?" Wao wakazidi kupaaza sauti: "Asulubiwe!" |
24 | Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, "Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe." |
25 | Watu wote wakasema, "Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!" |
26 | Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, lakini akamtoa Yesu asulubiwe. |
27 | Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima. |
28 | Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu. |
29 | Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, "Shikamoo mfalme wa Wayahudi!" |
30 | Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani. |
31 | Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. |
32 | Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu. |
33 | Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la kichwa," |
34 | wakampa mchanganyiko wa divai na nyongo. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa. |
35 | Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. |
36 | Wakaketi, wakawa wanamchunga. |
37 | Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lilioandikwa, "Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi." |
38 | Wanyang`anyi wawili walisulubishwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. |
39 | Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema, |
40 | "Wewe! Si ulijidai kulivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi shuka msalabani!" |
41 | Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria na wazee walimdhihaki wakisema, |
42 | "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Eti yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini. |
43 | Alimtumainia Mungu na kusema eti yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka." |
44 | Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana. |
45 | Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi yote ikawa katika giza. |
46 | Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eli, Eli, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" |
47 | Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, "Anamwita Eliya." |
48 | Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe. |
49 | Wengine wakasema, "Acha tuone kama Eliya anakuja kumwokoa." |
50 | Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho. |
51 | Hapo pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; |
52 | makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa; |
53 | nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika Mji Mtakatifu, wakaonekana na watu wengi. |
54 | Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, "Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu." |
55 | Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. |
56 | Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. |
57 | Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Armathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. |
58 | Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe. |
59 | Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya kitani, |
60 | akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. |
61 | Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi. |
62 | Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato, |
63 | Wakasema, "Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, `Baada ya siku tatu nitafufuka.` |
64 | Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa awali." |
65 | Pilato akawaambia, "Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo." |
66 | Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi. |